Leo tarehe 19 Oktoba 2019 kumefanyika mahafali ya 30 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Lwandai inayomilikiwa na Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, ambapo wanafunzi 119 (wa kike 60 na wa kiume 59) wamehitimu. Mgeni rasmi katika mahafali haya alikuwa ni Mhasham Askofu, Dkt Stephen Ismaili Munga aliyewakilishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Jamii, Mchungaji Joyce Kibanga. Mahafali haya yalifana sana yakipambwa na vishirikisho mbalimbali toka kwa wahitimu na wanafunzi wengine. Mchungaji Joyce Kibanga aliwaasa wahitimu kuendelea kujitahidi kusoma kwa bidii, na kwamba wazingatie maadili mema katika maisha yao. Mwisho aliwatakia baraka katika mitihani yao inayotazamiwa kuanza Novemba 4 2019. Awali katika hotuba yake, Mkuu wa shule aliwaomba wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule hii kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita ambapo vigezo vya kujiunga na kidato cha tano na sita ni ufaulu wa masomo matatu kwa kiwango cha alama C na katika masomo ya mchepuo wa chaguo lake asiwe na F.

Baada ya mahafali 30 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Lwandai Mkurugenzi wa Huduma za Jamii pamoja msafara wake walitembelea mradi wa usafishaji maji taka ambao umejengwa hivi karibuni. Huu ni mradi wa kwanza Tanzania na Afrika. Mradi huu umefadhiliwa na kujengwa na marafiki wa shule kutoka Ujerumani. Wajenzi wa mradi huu ni; Mhandishi Ralf Wagner akishirikiana na Mwalimu Edward Schnelein na Fundi bomba Bwana Michael Stroehlein.